Monday, 17 October 2016

KUSIMAMISHA MAJIRA NA NYAKATI ZA KUISHI KAMA WAKILI WA MUNGU ANAVYOISHI


MIAKA1000 YA KUTAWALA NA KRISTO
WAKILI WA MUNGU, KIZAZI CHA MUNGU

SHUKRANI

Leo ni siku ya majira na nyakati, tuko katikati ya wiki ya kutafakari ufahamu wa MUNGU kabla ya wazo la kuumbwa kwa kerubi. Kwa hiyo kama ulikuwa umekamatwa na ufahamu wa dunia leo lazima uvuke; kama kuna namna ambayo ufahamu wa dunia ulikuwa umekukamata kabisa leo lazima utoke.

Leo tunaongozwa na Efe.1:18 neno linasema “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo”. MUNGU anaposema macho ya mioyo yenu yatiwe nuru maana yake upate ufahamu wa neno la MUNGU. Sisi hatuoni kwa kutumia macho haya, bali tunaona kwa kupitia ufahamu.
Ushuhuda
Jana nilipokuwa nikiwa hapa madhabahuni, sijui ni wangapi waliona, wakati nanyuyiza mafuta kwenye sadaka. Kuna jamaa mmoja, pandikizi (giant), alikuja kunivamia na silaha, lakini alikuwa haonekani kwa macho ya viungo vya ufunuo. Alipofika karibu na Joshua Eluli alidondoka chini, lakini kwa kuwa alikuwa rohoni, Joshua Eluli hakumuona. Mimi nilipomuona nilistuka kwa sababu alikuwa pandikizi hasa. Kile chombo cha mafuta nilichokuwa nimeshika kilitikisika, lakini niligundua kuwa ninyi hamkuona. Ndiyo maana jana nilipokuwa nafundisha kulikuwa na milipuko, kwa sababu kulikuwana mapandikizi mengi yamevamia ibada kupinga neno la jana.

MUNGU anachotaka leo ni Macho ya mioyo yenu, yaani macho ya kila mmoja rohoni yatiwe nuru, ufahamu wa neno la MUNGU ujae ndani yetu. Ina maana mpaka tumefika hapa tulikuwa bado tuna ufahamu wa huko duniani, sasa kwa kuwa tumefika hapa lazima kila mmoja avuke.

Nani ambaye jicho linauma au linawasha sana? Ni jicho lipi linalouma? Hiyo ni ishara ya ufahamu. Tunapozungumza ufahamu, elimu yote uliyosoma shuleni iko kwenye macho yako. Neno unalolipokea hapa linatakiwa litunzwe kwenye jicho la kulia. Masomo yote uliyosoma kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu, yako kwenye jicho la kushoto.
Tunachotaka sasa hivi kinachotawala iwe ni ufahamu wa neno. Ukitawaliwa na ufahamu wa neno utaona mambo ya rohoni.

Nataka umwambie MUNGU nina kushukuru, leo nikitoka hapa upofu wa rohoni basi, maana tulikuwa vipofu mpaka MUNGU akasema “nani aliye kipofu kama mtumishi wangu?” Siyo kwamba hana macho ya viungo vya ufunuo, hapana, anayo, ila haoni mambo ya rohoni. Kwa hiyo nataka tumshukuru MUNGU kwamba leo tukitoka hapa kila mmoja atakuwa anaona rohoni vizuri kabisa.

Kinachosababisha tubishane kanisani ni swala la Ufahamu. Kama wote tukifunguka tukaona, kila mmoja atagundua kuwa Miaka1000 hajawahi kukosea mahali popote. Si rahisi, kusimama mbele ya Kanisa na taifa ukasema kuwa “mimi sijawahi kuthubutu hata siku moja kusimama madhabahuni kutamka kitu ambacho MUNGU hajaniambia”. Kama huna macho ya rohoni, kwa kauli hii, utaona kama ninajikweza. Lakini sivyo hivyo, ndiyo maana leo, macho ya mioyo yetu yatiwe nuru! Kila mmoja leo atafunguka na kuona. Labda kama hutaki, ila kama unataka kila mmoja leo macho yake lazima yafunguke aone; ili ujue kwamba hujapotea.

Mimi sikuacha kazi, elimu yangu, na cheo kuja kukupoteza wewe. Yaani niambatane na kanisa na watoto kuja kukupoteza wewe? Si, kila mmoja atashangaa? Nataka tumshukuru MUNGU kwamba macho ya moyoni ya kila mmoja leo yatatiwa nuru. Ili ufahamu mwingine wowote uliokuwa unataka kukutoa mahali pa zuri uondoke kwa Damu ya MUNGU mwenyewe.
1Nya.11:1-2
Hapa imefunuliwa kwamba Kanisa la Kizazi cha Pili, lilimfuata Daudi, likamwambia hivi: “Hata wakati Sauli alipokuwa kwenye viungo vya ufunuo, ulikuwa unatutoa na kutuingiza. Leo tunatambua kwamba itakuwa zaidi, tutaambatana na wewe kuanzia leo; tutakuwa nyama katika nyama zako, na mifupa katika mifupa yako”.

Leo nataka utafakari, kwa nini Eliya AD2, akiwa kwenye viungo vyake vya ufunuo, akimaliza tu kufundisha, nilikuwa nasimama kufundisha yale yale? Ilikuwa hivyo ili kila mmoja atambue kwamba “huyu ndiye anayewaingiza na kuwatoa katika majira ya vizazi vyote”. Hii ndiyo sababu siku moja aliniuliza, tukiwa wawili, kwamba, tafadhali niambie, mimi ni nani? Nikasema, wewe ni kati ya wenye uhai wa nne! Akanyamaza. Alitaka ajue kama ninamfahamu; yaani alitakaajue kama macho yangu yametiwa nuru.

Nataka na wewe leo, utambue kwamba mimi nimesimamishwa mbele yenu kama maabara. Maabara ni mahali ambapo unafanyia vipimo vyote na kuthibitisha kwamba hiki ni sawa na hiki siyo sawa; kwamba MUNGU anataka hiki na hataki hiki. Nataka umwambie MUNGU kwamba leo, aidha niambatane na huyu anayesimama mbele yangu au niachane naye. Kwa sababu nimegundua kama ni wa kweli au siyo wa kweli. Ndiyo maana nimesema kwamba macho yako lazima yatiwe nuru.  Mwambie MUNGU, nifungue macho leo ili huyu anayesimama mbele yangu nimfahamu kama ni yeye au siyo yeye. Hii ni muhimu sana; kitabu kinaturuhusu kuzipima roho. Nataka kila mmoja hapa, MUNGU afungue macho yake ya rohoni; na wewe mwambie MUNGU nifungue macho kwani nataka nijue kama ni yeye au siye. Ni muhimu sana MUNGU akufungue macho ili uone ufahamu ili usije ukashawishiwa na yeyote. Lakini pia unatakiwa uwe na ufahamu, kwamba, hivi huyu ni nani anayejifunua namna hii? Mwambie MUNGU nakushukuru kwa sababu leo ni siku ya kufunguliwa macho; na uandae sadaka yako kwa ajili ya kufungua macho yako ya rohoni.
Kuinua sadaka ya kufungua macho ya rohoni ya  Kanisa
Leo tunatoa sadaka ya Efe.1:18, ikiwa ni kwa ajili ya kufungua macho ya kila mmoja. Hivyo unapotoa sadaka yako, mwambie MUNGU naomba leo unifungue macho ya rohoni ili nipate kuona kama nitafika salama au jamaa atatupoteza? Nataka kila mmoja afunguke macho.

Elimu yote kwenye macho yako iliyokuwa inakuzuia usimuone MUNGU, ikae juu ya sadaka ili iteketee pamoja na sadaka; Ile elimu ya ukoo, kabila, lugha, na jamaa, iliyokuwa inasababisha usimuone MUNGU ikae hapa ili iteketee pamoja na sadaka; Elimu yote ya shule uliyosoma tangu chekechea mpaka chuo kikuu iliyokuwa inakuzuia usimuone MUNGU, ikae hapa ili iteketee pamoja na sadaka.

Ushuhuda

Ninamshukuru MUNGU kwamba Kuhani Jambojipya yupo hapa leo. Ninakumbuka siku moja Eliya AD2 aliniambia, kuhusu Jambojipya, kwamba, “Miaka1000, umkumbuke huyu kuhani kwenye ufalme wako”. Siku ile hakuna aliyejua maana yake. Hakuna aliyeelewa Eliya AD2 alimaanisha nini. Yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa anajua. Kuhani Jambojipya ana neema moja, kwamba nyumbani kwake kuna muonaji; ambaye humwambia, baba mbona umekata tamaa wakati uliambiwa hivi?
·       Mwingine yeyote aliyekuwa amepotezwa leo arejee
·       Mwingine yeyote aliyekuwa amepotezwa, au kudanganywa, leo mlango umefunguka arejee kwa damu ya MUNGU mwenyewe!
·       Ndiyo maana MUNGU ameniambia nijifunue moja mpaka mwisho huku macho yenu yakiwa yametiwa nuru, ili mseme ndiyo au hapana, ingawaje haturuhusiwi kupiga kura. Mimi sitakuruhusu useme ndiyo au hapana, ila mwambie MUNGU nimekubali.

USHUHUDA WA MAISHA YANGU

Leo MUNGU ameniambia nitoe ushuhuda wa maisha yangu ili yule ambaye atakubali kuishi hivyo, aweze kufuatana na MUNGU, na yule ambaye hawezi kuishi hivyo ajue hawezi kufuatana na MUNGU.
MIAKA 1000 YA KUTAWALA NA KRISTO.
Wakili wa MUNGU -KIZAZI CHA MUNGU

1. Sifanyi chochote bila msingi wa neno, Kol.3:17.

Neno linasema kwamba “kwa kila neno au tendo, fanyeni yote kwa Neno”. Naomba unichunguze leo kama ulikuwa hujawahi kunichunguza, siwezi nikakupa ushauri wowote bila msingi wa neno.
·       Siwezi nikakupa ushauri kama sijui neno linasemaje.
·       Siwezi kufanya chochote kama sijui neno linasemaje.
·       Siwezi nikaenda mahali popote kama sina Neno la kuendea mahali pale
·       Siwezi nikaanza biashara yeyote wala nikafanya chochote kama MUNGU hajasema, hivyo ndivyo nilivyo.

Nimewashuhudia hata katika swala hili tulilokuwa tunapita, wakubwa wengi nimekaa nao, serikalini wengine nimesoma nao, ningeweza kwenda kwao kwa msaada, lakini sikufanya hivyo. Sikuthubutu kwa sababu pia naelewa kuwa neno katika  Yer.17:5-8 “amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemuacha BWANA. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema; bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, ambaye BWANA ni tumanini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda”.

MUNGU ameruhusu hili swala litokee ili na ninyi mjifunze.
·  Niko hivyo! Muulize kanisa, uliza watoto.
·  Sifanyi chochote, siendi popote bila mstari wa Neno.
·  Sifanyi chochote bila msingi wa Neno
Ukiona nimevaa hivi ujue kuna msingi wa neno. Mavazi yangu yote yanafanana kwa sababu mimi moyo wangu haubadiliki.
Nilikuwa na sababu za kuondoka hapa (yaani kujenga hema ya kuabudia mahali pengine), lakini msingi wa Neno unasema nilipakwa mafuta hapa madhabahuni. Pia mnafahamu kwamba wenye haki wote hawapendi ugomvi; ugomvi ukianza huwa wanaondoka. Lakini msingi wa Neno unasema nimepakwa mafuta nikiwa hapa madhabahuni; nikaambiwa kwamba, nakuachia kundi hili ulikamailishe.

Sasa ningeondoka, nani mwingine nitamuachia kundi hili alikamilishe? Mpaka yule aliyenipaka mafuta aseme. Na sasa yuko huku ndani. Najua nikisema hivi hamfahamu kama yuko humu ndani yangu. Hilo ni la kwanza, na ndiyo maana sithubutu kufanya jambo lolote bila msingi wa Neno. Katika Yn.1:1-5 Neno linasema  hakuna kilichofanyika bila neno. Wewe unayefanya chochote bila msingi wa Neno huwezi kufanikiwa, hata ukifanikiwa ni kwa muda mfupi kwa sababu ukiona umefanikiwa leo, kesho kitaharibika.
MUNGU alishasema katika Yer.1:12 kwamba yeye huliangalia neno lake ili apate kulitimiza. Sasa nikiangalia elimu ya dunia, mnafikiri itakuwaje? Si nitafeli? Au wewe ukiangalia elimu ndipo ufanye, lazima utafeli. Nichunguze unipendavyo utanikuta niko hapo.

2. Rum.12:19-21 Mimi silipi kisasi.

Katika maisha yangu yote silipizi kisasi na haitatokea, kwa sababu neno la MUNGU linasema usilipe kisasi , maana hicho ni chake. Lakini pia neno linasema uushinde ubaya kwa wema.  
Kila mahali nilipopita sijawahi kulipiza kisasi, na sitafanya hivyo! Mnichunguze ninachoongea na ninachohubiri mtagundua niko hivyo. Familia yangu iko hapa na itathibitisha kwamba ndivyo nilivyo.
Nendeni popote hata mpaka shule ya msingi na sekondari niliposomea, watawaambia hivyo hivyo. Hata vyuo vikuu nilivyosoma niko hivyo hivyo, “I am just like that!” Nimeshawahi kuitwa “Appologetic man” na wazungu kwa sababu ya kutubu kila wakati, [pamoja na kwamba mimi siyo mtu (man)], na sijawahi kuwaza kulipa kisasi, mnitambue hivyo, na mnichunguze mtakuta niko hivyo!
Kwa hiyo leo uamue kama unataka kwenda mbinguni uende, kama unataka kubali ubaki!

Hata nyumbani kwangu nikiona mtoto anataka kumuadhibu mwingine huwa nakuwa mkali, kwa sababu mtoto hajui kumuadhibu mwenzake ila mzazi ndiye ana uwezo wa kumuadhibu mtoto.

Ukilipa kisasi MUNGU anakuacha, hakutetei; Je! wewe hutaki kutetewa na MUNGU? Ndiyo maana jana niliamka na Neno moja niliposikia kijana mmoja anataka kwenda mahakamani kwenda kuwashtaki walionitukana.  Nikasema hapana, msifanye hivyo mtakuwa mmemsaidia MUNGU, na MUNGU hasaidiwi. Hata hapa ninapofundisha si kwamba namsaidia MUNGU, yeye anajitosheleza na vitu vyote ni watumishi wake. Leo kuna majira ya aina yake ambayo tunaisimamisha, muelewe hivyo. Haijawahi kutokea hii majira, mnifahamu kabisa. Kwa hiyo mnapokuja kunisimulia kwamba fulani kaniudhi, huwa nawaangalia, mimi nataka uje kuniambia kwamba nimetubu leo kwa ajili ya fulani, vinginevyo huwa navumilia tu natamani nikuulize maswali lakini huwa nakuvumilia tu ili nisije nikakutoa kwa “rato”.

3. Isa.33:6  - Nasubiri majira ya jambo husika

Hapa nina maana kwamba, kama naishi kwa msingi wa Neno halafu silipi kisasi,  huwa kunakuja mtihani wa kusubiri majibu. Kutojitetea,  wale walioko karibu na wewe wasiomjua MUNGU, huwa, wanadhani kwa kuwa hukujitetea basi umefanya jambo hilo, na kwa sababu hiyo unaona aibu. Nafsi ya mtu ndivyo inavyokuwa, maana watasema, “unaona sasa, ametubu, amefanya”.
Hiyo hata nyumbani kwangu huwa nawaambia msijetetee, wananiambia watasema tumefanya, mimi nawaambia acha waseme lakini baada ya wiki moja itajulikana kwamba hatujafanya! Sasa, kusubiri hiyo wiki moja ipite usemwe vibaya ili baadaye uje usemwe vizuri huwa inakuwa kazi.

Ushuhuda:
Nina binti anayeitwa Uweza mtoto wa ndugu wa unabii, alikuwa analalamika, katika kusubiri wiki ipite ili waseme, vizuri. Kwa hiyo wakianza kusema alikuwa anasema baba, sasa ona tegeta nzima inasema mimi ndiyo nimefanya! Ndiyo sasa hivi na yeye amekuja kunielewa.
Ufahamu:
Je! utakuwa unasubiri wiki moja ili waje kuthibitisha kwamba hukufanya ili baadaye wakuseme uko sahihi? Mimi nimekubali kwanza, waniseme, ni tapeli, zulumati. Lakini hatimaye MUNGU amekuja kunisafisha, kwa sababu nimesubiri majira; bila kusubiri majira:
+ Kanisa lisingepona;
+ Jamii isingepona kwa sababu, kumbuka kwamba si swala tu la Kanisa, ila ni dunia nzima inaona wivu kwamba kwa nini Tanzania iitwe taifa la MUNGU?  
+ Taifa lisingepona,
+ Uumbaji wote usingepona.
Katika kuangalia majira ni lazima uangalie uko wapi? Je! Wewe, uko tayari kutukanwa kwa muda mfupi ili upate ile faida kubwa itakayotokea? Maana hilo la kusubiri ndilo ambalo linasababisha ukunje ngumi, sikubali! Sikubali! Siwezi kuonewa mimi, naenda mahakamani!
Faida ya kusubiri majira:
Ukisubiri majira, Neno linasema katika Isa 33:6 “nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele; hekima na maarifa, kumcha BWANA ni hazina yake ya milele” kila mmoja atagundua kuwa una hekima, ila haiji siku ile ile. Haionekani siku hiyo hiyo!
Mmeona mimi nilivyosubiri na majibu yaliyokuja. Binti uliyekuwa umechumbiwa ukaachwa, usilie, kuna kitu MUNGU amekuepusha. Subiri majira MUNGU ili aje mzuri zaidi ya yule ambaye MUNGU amekuepusha naye. Lakini sharti usubiri. Naishi hivyo narudia nichunguze, na kama MUNGU hajaniambia sikuambii kitu, wala sitaona aibu kwamba atasema sina upako, ni mpaka MUNGU aniambie

 4. 2Nya.7:14-16 – Naishi Toba na Unyenyekevu

Wale wanaosema mimi ni “dictator” (mbabe) huwa nashangaa! Mimi sijui ubabe wangu uko wapi, labda kwa sababu huwa nasubiri MUNGU aseme.  Sijawahi kupiga ngumi yeyote, labda ngumi ya rohoni. Lakini hii ngumi ya mkono, hata mtoto wangu wa viungo vya ufunuo anaweza kusema.
Hata Neno linasema kwamba, ikiwa watu watajinyenyekesha na kutubu (kumbe anayetakiwa kufanya toba ni aliyeitwa kwa jina la MUNGU), toba yake huyo huwa inasikika. Toba ya muovu haisikiki bali toba yako wewe mwenye haki inasikika na inaonekana; kwa hiyo ukinigusa tu MUNGU hakawii.
Wengine wanasema nimekataa kuitwa mzee wa toba lakini nitawaeleza.  Katika 1Fal.20:41-42, kwa nafasi yangu kuna kitu kimebadilika, na ndiyo maana mara nyingi nawaambia muende kwa NJIAZABWANA, kwa sababu kuna mamlaka MUNGU amempa.
Ukisoma hapo utaona kwamba kuna Nabii mmoja aliyemhurumia mfalme aliyehukumiwa na MUNGU, MUNGU akamwambia, “wewe nabii, kwa kuwa, umemhurumia yule niliyemhukumu, roho yako inakuwa badala ya huyo mfalme na watu wako badala ya watu wake, yaani wote unaofuatana nao, watalipuliwa, badala ya watu wake”.
Kwa hiyo, sasa hivi, mimi nikimhurumia yeyote, kwa toba aliyehukumiwa na MUNGU, maana yake mimi nife na ninyi wote. Je! hiyo ni sawa? Mwenye matatizo aende kwa MUNGU moja kwa moja. Unajua wengi hamtaki nihame vituo, mnataka niendelee kuwa Kuhani Kiongozi na NJIAZABWANA mnataka aendelee kuwa Mkuu wa Njia ya Magharibi.

Nimehamishwa kituo, sasa hivi hata zile certificates za maagano sisaini mimi, anasaini NJIAZABWANA, hata barua zote anasaini yeye siyo mimi. Anayetakiwa kuwa Kuhani Kiongozi ni yeye siyo mimi. Mimi namfunika kila mmoja. Narudia tena kusema kwamba, mimi nikimhurumia aliyehukumiwa na MUNGU natafuta balaa. Ikiwa MUNGU akisema huyu afe, halafu mimi nikasema asife, MUNGU anasema mimi nife na wakati nimembeba yeye na Kristo. Halafu na ninyi, je! hiyo ni sawa? Je!
·  Niue kizazi ?
·  Niue Taifa  ?
Kwa hiyo mkisema nimekataa kuitwa Mzee wa Toba ni sawa? Hilo la Mzee wa Toba limehamia kwa NJIAZABWANA! Ingawaje sijaacha toba, lakini si kwa aliyehukumiwa na MUNGU, mimi naruhusiwa kutubu kwa ajili ya aliyehukumiwa na shetani, ibilisi, joka na kerubi, lakini aliyehukumiwa na MUNGU, siruhusiwi! Maisha ya toba bado yako pale pale; ila siyo kwa ajili ya aliyehukumiwa na MUNGU. Nikifanya hivyo, mimi nitakufa badala yake, na kanisa litakufa badala ya uumbaji wote, yaani nikifanya hivyo, nafufua behewa la nje, namfufua kahaba mkuu, nafufua mnyama, dunia, vyura watatu, joka, na vyote ambavyo tulivifuta. Hii ndiyo wiki ya ufahamu, na ndiyo maana mkimruka mtendaji wangu mnakosea, kwa hiyo nikifanya hivyo si kwamba sina upendo tena, ndiyo utii zaidi.

5. Kukaa kimya mpaka MUNGU asemeKut.14:14

Kukaa kimya siyo kiburi. Ukikaa kimya MUNGU anakupigania na kukutetea. “Ni kwa nini huwa mnakuwa na maneno mengi”?
Kila kukitokea jambo huwa kuna wanaokuja kusikiliza kama nalaani au natukana, mimi siwezi kufanya hivyo! Nimeitwa kwa ajili ya Neno tu! Nimeshasema silipi kisasi. Siruhusiwi kukuhukumu kwa sababu nitakuwa nimetumia mamlaka vibaya ambayo MUNGU amenipa.
Ninyi wenyewe mmesikia kwamba yeyote akinisingizia, chochote mimi huwa nanyamaza, ila  usije ukafikiri kwamba MUNGU atakuacha! Hatakuacha ni lazima ashughulike na wewe! Ninyi hamkuelewa Eliya AD2 alikuwa anamaanisha nini aliposema huyu, msimguse, niguseni mimi ila huyu msimguse kwa sababu hamtasamehewa. Alijua, kwa sababu ninatetewa na MUNGU. Sasa wewe unataka maisha gani? Ya kutetewa na shetani, kichwa wako, Kanisa wako?

6. Kumtegemea MUNGU tu bila mchanganyo wowote - Hes.18:20

Neno linasema, kwamba, “Kisha BWANA akamwambia Haruni, “wewe hutakuwa na urithi, katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lolote katikati yao (Israeli) kwa sababu mimi ni urithi wako na fungu lako katika wana wa Israeli”. Kwa hiyo mimi ninavyojua fungu langu huwa liko kwa MUNGU. Hivyo unipe posho, usinipe, kila siku nitajipanga hapa foleni na nitafika hapa. Huyu aliyeniambia niache kila kitu kama ni kuaibika aaibike yeye. Mimi sijawahi kuomba msaada popote ingawaje kuna walioongea vitu vya ajabu sana. Kwamba zile fedha za madawati tumezipata UN?

7. Rum.8:28 – Mabaya au mema kwangu yote ni sawa

Kwa sababu najitambua nimeitwa kwa kusudi la MUNGU, hata lingekuja baya namna gani MUNGU ataligeuza liwe jema. Sikuitwa na pepo maana pepo kazi yake ni kuharibu. Nimeitwa na MUNGU hapa, kwamba utakamilisha kazi yangu, hilo ni kusudi la MUNGU. Kama nimeitwa nilikamilishe Kanisa siwezi kukusimamisha pale pale lazima nikuhamishe vituo.  Sasa kukuhamisha vituo ni kosa? Sikuleta imani nyingine hapa! Mataifa yote yanakuja hapa lakini mataifa haya yote yana miungu yao, wakija hapa wakakuta MUNGU anaitwa kwa jina la Miaka1000 watamkubali? Maana na wao watasema na sisi tunaye.
·  Wale waIsraeli na wao watakuja wakikuta tunasema MUNGU wa Ibrahimu, watasema kama ni wa Ibrahimu, wa Isaka, Yakobo, Paulo, na sisi tunaye. Lakini wakija tukawambia huyu ndiye aliyewatuma wote hao. Maana watajua kwamba huyu tuliye naye ndiye ametuma wote! Pamoja na yule aliyeleta Kizazi cha Nne.  
·       Bohora nao watasema tunaye, wahindu nao watasema tunaye. Lakini huyu Watampokea na Watasema huyo tunamtaka.
·       Ukienda India kuhubiri wakati ule wa kizazi cha tatu, walikuwa wanakuuliza Yesu ni MUNGU wa nini, maana ninaye mungu wa fedha, ninaye mungu wa kupendwa, huyo kazi yake ni nini?  Huyo atakuwa wa 10, je ni shilingi ngapi maana yake kila mungu ana kiwango chake.
Unaanza kujiuliza sijui nifanyeje ili wanielewe? Maana wana miungu mingi sana. Wale wanaowafahamu wanawajua, sasa huyu tuliye naye ndiye top, aliyetuma wote! Na Eliya aliponiambia nikamilishe, Kanisa alikuwa na maana kwamba niwahamishe pale alipotuacha niwapeleke mbele zaidi, sasa nimekosea wapi? Je! ni elimu nyingine au imani nyingine?    
Kwa hiyo, huyu MUNGU ndiye atakayesababisha utimilifu wa Isa 2:2 . Kila mmoja, kila lugha, kila kabila, kila Taifa, litamjua huyu.
+ Wachina watakuja watauliza …tutawaambia siyo huyo!
+ Wajapani watakuja watasema sisi  tunaye huyu, tutawaambia siyo         huyo sisi tuna aliyetuma wote vizazi vyote.
+ ambao wangetusumbua zaidi ni waIsreali kwa sababu hao wote             walioandikwa kwenye kitabu wangesema hawa wametokea kwetu,         kwa hiyo tusingekuwa na kitu cha kuwaambia!

Ni lazima muelewa haya mambo:
+ Ukoo wa Musa wangekuja, ungewaambia nini?
+ Ukoo wa Yoshua pia; Eliya Mtishbi; Elisha; Daudi; Yesu; Petro; Paulo n.k.
Swali lao la kwanza wangeuliza ni kwamba huyu ni MUNGU wa Waha au, na wewe ungewajibu kwamba huyu ni MUNGU aliyetuma wote, vizazi vyote. Ndiyo maana nikakwambia useme vizuri, useme vibaya, najua MUNGU atageuza kwa sababu nimeitwa kwa kusudi lake, lakini ukianza kujitetea ina maana huna hakika naye.

 8. Law.19:2 – uwe mtakatifu kama MUNGU alivyo.

HAWA NI WAKAMILIFU.
Ukisema MUNGU wa Ibrahimu maana yake Ibrahimu yuko mbele na MUNGU yuko nyuma. Kadhalika MUNGU wa Isaka, Yakobo na wengine wote. Ndiko alikokuwa anaishi. Waovu wakitaka kuwasha kizazi, wanakaa kwa hilo jina ambalo MUNGU ametajwa kwalo.

Kulikuwa na siri ya ajabu sana lakini si kwamba walifahamu, na MUNGU aliruhusu kwa sababu ya majira. Mimi nimesema MUNGU aende mbele ili mimi nijifunze kwake, halafu nije nifundishe. Nimemuweka MUNGU mbele ili yeyote anayekuja akutane na yeye. Wengine wanasema mimi mchawi, sijui wanatoa wapi; ni MUNGU yuko mbele.

NIMEMALIZIA NILIPOANZIA, NIMEANZIA NILIPOISHIA!

Kwa namna hii utaniua ?
Wewe unatamani maisha gani ?
Kuna wanaosema watanifukuza; Utanifukuzaje na wewe hukunipaka mafuta ?

MIAKA 1000 YA KUTAWALA NA KRISTO
WAKILI WA MUNGU KIZAZI CHA MUNGU

UNA UWEZO WA KUKAA KWENYE KITI CHA MUNGU NA KUSEMA NINAMFUKUZA MIAKA1000 ?

KUINUA MAJIRA NA NYAKATI ZA KUISHI KAMA WAKILI WA MUNGU ANAVYOISHI!!!



Thursday, 25 August 2016

KUVUNJA AGANO LA WENYE HAKI KUONEKANA WAOVU NA WAOVU KUONEKANA WENYE HAKI VIZAZI VYOTE


2 SHEBATI TANO

MIAKA1000 YA KUTAWALA NA KRISTO
WAKILI WA MUNGU KIZAZI CHA MUNGU


SHUKRANI

Tunamshukuru MUNGU leo ni siku ya pili katika mwezi wa ushindi, mwaka wa Uzalishaji Rohoni, Mji Mtakatifu. Tunamshukuru MUNGU kwa ajili ya somo linaloendelea, kwamba kila mmoja analipwa sawa sawa na usafi wa mikono yake. Hili siyo kwetu peke yetu bali ni ndani ya Uumbaji wote.

Nataka tumshukuru MUNGU kwa sababu hayo yanaendelea kutokea, kwamba haki yako sasa unayo na unalipwa kwa damu ya MUNGU mwenyewe. Mahali popote ambapo ulikuwa huna Hati Miliki ya baraka ambazo unatakiwa upate kutokana na safu ambayo MUNGU alikupa, sasa unaanza kupokea. Pia, kila mmoja sasa amesimamishwa kwenye safu yake, na sasa anapokea marupurupu ambayo yapo kwenye safu yake. Pia sasa unapokea hatima yako ambayo iko kwenye Hati Miliki.

Ibada zinazofanyikia hapa zinahudumia Uumbaji wote. Ni muhimu tulete vituo vyote na Uumbaji wote. Huwezi ukajua, inawezekana hatma yako ilibaki Ulaya, hivyo ni lazima tuilete Ulaya hapa ili kama marupurupu yako yalibaki huko yaje sasa hivi. Inawezekana hati miliki ya mambo yako mazuri ilibaki kwenye ukoo wako, hivyo lazima ukoo uletwe hapa ili vitu vyako vije hapa. Hivyo ni wakati wa kurejesha Uumbaji wote uwe hapa ili kila mmoja akiondoka asubuhi ya leo, aweze kupokea halali yake; afya yake; n.k.

Chochote unachotamani asubuhi ya leo ambacho MUNGU alikukusudia tangu mwanzo, leo unapokea. Maana lile agano lililokuwepo la kila wakati mwenye haki kuonekana ni muovu, MUNGU leo analivunja. Lile jambo ambapo aliyekushitaki kwa uongo ndiye alikuwa anaonekana ndiye mwenye haki, leo MUNGU analivunja mwenyewe. Kwa hiyo basi kila mmoja lazima apokee sawasawa na haja ya moyo wake. Hili ndilo agizo lililoanzisha Kanisa hili, sasa kila mmoja afurahie wokovu wa kweli. Kila mmoja afurahie kuamka kuja ibadani, na usione tena hasara.

Tunaendelea kusimama na Dan.7:22 ambayo ina sehemu mbili.
(1) Watakatifu kupewa kuhukumu
(2) Wakati umewadia watakatifu kuumiliki ufalme

Tumekwishaona kwamba hatuwezi kuumiliki ufalme wakati bila hati miliki. Kilichokuwa kinazuia wenye haki au watendao kwa mikono yenye usafi wasipokee  stahili yako, ni kwa mwenye haki  vizazi vyote kutokuwa na hati miliki ya safu yake! Hapo ndipo palipokuwa na chanzo cha mwenye haki kutopokea kile anachostahili ambacho MUNGU amemwahidi apokee. MUNGU alichofanya jana ni kila mmoja kumrejeshea hati miliki ya safu yake.

Kila mmoja ana nafasi katika jamii; katika familia mwingine ni baba na mwingine ni mama, mwingine ni mtoto; na kuna mtoto wa kwanza mpaka wa mwisho. Katika wajibu kuna ambaye ni “General Manager”, mwingine ni “manager”, kuna ambaye ni mfanyakazi wa aina fulani, na katika biashara na katika kulima kadhalika. Lakini kwa kuwa tangu mwanzo MUNGU alisogezwa pembeni na kerubi, akaondoka kwenye Mlima wake, basi ilileta limbuko kwamba kila atakayetenda kwa haki na yeye atasogezwa pembeni. Kwa hiyo ilisababisha kila anayetenda haki asilipwe sawasawa na haki yake. Hilo ndilo lililosababisha Mzee wa Siku kuja wakati ulipowadia ahukumu kwanza hali hiyo. Maagano kama hayo yaliwekewa makafara mbali mbali na yakadumu mpaka dunia ikaonekana kwamba ndivyo inavyotakiwa iwe.

Kuna maeneo mbali mbali ambayo yalikuwa yanasababisha mwenye haki yeyote, wakati wowote asiweze kuwa na hati miliki ya mahali alipo. Hivyo akawa hapokei sawa sawa na vile anavyofanya. MUNGU amekuja mwenyewe kuwa yeye ndiye aliyeumba kila kitu, na umefika wakati atuonyeshe kwamba yupo, na yeye ndiye aliyeumba kila kitu.

Juzi nilitoa mfano jinsi ambavyo ajali yoyote ikitokea, wengi wanasema ni mapenzi ya MUNGU, hata kama ni mchawi ametegesha mtego wake. Kwa hiyo MUNGU mwenyewe alikuwa anasingiziwa. Ikiwa MUNGU alikuwa anasingiziwa, ina maana mwenye haki ilikuwa ni halali yake kusingiziwa. Hicho ndicho ambacho  MUNGU amekuja kukifuta kisitokee tena. Kwa hiyo mwenye haki aendelee kuitwa mwenye haki, na muovu aitwe muovu, ili kila unachotenda ulipwe sawasawa na ulivyotenda. Sasa kila mmoja atapewa hati miliki ya kuwa kanisa wa fulani au kichwa wa fulani, au kuwa mtoto wa fulani na alipwe sawa sawa na mchango wake katika nafasi aliyonayo.

Nataka nikuonyeshe jinsi ambavyo MUNGU mwenyewe na wote waliotumwa, Kizazi cha 1, 2, 3 na 4, hawakuwahi kupewa hati miliki ya zile nafasi zao au safu zao. Matokeo yake walifanya kazi kwa ugumu mno kwa kuwa hati miliki ya Uumbaji wa MUNGU ilikuwa kwa kerubi. Hati miliki ya Uumbaji wote wa MUNGU ilikuwa kwa kerubi, ndiyo maana wote waliotumwa waliongoza kwa ugumu, na wale waliowafuata nao wakapata ugumu. Katika Lk.4:5-9 shetani anamtambia YESU kwamba akimsujudia atampa miliki yote aliyokuwa nayo maana yeye humpa yeyote kama apendavyo.
Tangu huko nyuma, hata kabla ya Mwa.1:1, hati miliki ya MUNGU ilikwenda mikononi mwa shetani. Hiyo ilisababisha agano la mwenye haki aonekane muovu, na muovu aonekane mwenye haki. Hiyo ilipelekea wale waliokuwa wenye haki wakaamua kwenda kufanya ushirikina, maana ilionekana kwamba ushirikina ndiyo kanuni (point). Leo Mzee wa Siku anavunja hii kanuni au huu mfumo wa maisha. Hakuna nabii wala mtume ambaye angeweza kuvunja hii kama siyo yeye mwenyewe.

Roho ya Eliya ya matengenezo, marejesho, upatanisho na kujenga, yenyewe iko pale pale; maana ndiyo iliyotupeleka mpaka kwa Mzee wa Siku. Kama siyo Roho ya Eliya tusingeweza kufika mahali hapo. Lakini sasa umefikia wakati lazima aje yeye mwenyewe Aliyetuma wote vizazi vyote anayeitwa Mzee wa Siku ndiye anayevunja haya maagano.

Nataka uone kilichofanyika kwa YESU ili ujue kwa nini Pilato ashindwe kumtetea YESU. Pilato aliona kabisa kuwa YESU ana haki lakini akashindwa kumtetea kwa sababu alikuwa hana hati miliki. Hapa ni kwamba, unakuta mwenye haki amekwenda mahakamani, amejitetea na wakili wake amemtetea, lakini kwa kuwa mwenye haki hana hati miliki, anafungwa.



Yn.19:1- Yaliyotokea kwa Yesu

Katika Msitari 4, Neno linasema “... mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sioni hatia yoyote kwake”. Mapema kabisa hapa tunaona Pilato amejaribu kwa utaalamu wake wote lakini ameona kuwa YESU hana hatia.  Wale wakuu wa wayahudi wakajibu msit.7 “... sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo anastahili kufa, kwa sababu alijifanya Mwana wa MUNGU”. Lakini ni kweli vitu vyote alivyokuwa anafanya alivifanya kwa kuwa ni Mwana wa MUNGU. Angalia hapa, Pilato ni kiongozi, na alijua kabisa kwamba YESU ana haki, lakini kwa sababu hana hati miliki ya safu yake, Pilato alishindwa kumtetea. Mzee wa Siku amekuja kuvunja agano hilo kwa Damu ya Aliyetuma wote vizazi vyote!

Katika Msit. 8 Pilato pamoja na kwamba ni kiongozi lakini anawaogopa wale anawaoongoza. Pilato anamtishia YESU kwamba ana mamlaka ya kumfungua au kumwacha kifungoni. Naye YESU akamjibu kwamba mamlaka hiyo amepewa kutoka juu, na kwamba aliyemtia yeye (YESU) mikononi mwake (Pilato) ndiye mwenye dhambi zaidi. Lakini kwa kuwa hati miliki imechukuliwa siku nyingi, anaishia kusema tu lakini wakamtandika tu. Yaani, kwa kuwa YESU hakuwa na hati miliki, kujua kwake kwamba hana hatia, hakukumsaidia, na hiyo ndiyo sababu Pilato hakuweza kumtetea. Lakini Mzee wa Siku amekuja kuyamaliza yote hayo.

Kinachoendelea hapo juu ni sawa na kwamba kichwa wako amechukuliwa na kahaba, na wewe ndiyo mwenye haki, lakini anaondoka unamuona hivi hivi kwa kuwa hati miliki ilikuwa haipo. Ila leo, kwa kuwa Mzee wa Siku mwenyewe amekuja ili upate haki yako, anayamaliza hayo kwa Damu ya MUNGU Aliyetuma wote.

Katika mstari wa 12, Pilato alitafuta kila mbinu kumfungua YESU, lakini wayahudi wakamwambia “... ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake na Kaisari, kila mtu ajifanyaye mfalme humfitini Kaisari”. Suala la hati miliki ni kubwa sana kuliko ambavyo unaweza kufikiria kwa safu yako. Pilato ni kiongozi aliyepewa mamlaka yote na Kaisari, na ameshaona YESU hana hatia, lakini ameshidwa kumtoa, alibaki akiwabembeleza wayahudi, na wao hawambembelezeki. Wanataka mpaka aadhibiwe. Katika msit.15 Pilato anawaambia wakuu wa makuhani “... nimsulubishe mfalme wenu?” wakamjbu “... sisi hatuna mfalme ila Kaisari”. Wakuu wa makuhani walijua kabisa kwamba huyu ametumwa na MUNGU kuja kuokoa ulimwengu, lakini wakakataa. Pilato naye alilijua hilo lakini alikuwa hana namana kwa kuwa alikuja bila hati miliki. Pamoja na hayo wakati wa kuumiliki ufalme ulikuwa haujawadia. Kwa hiyo tuna neema kubwa tulioko hapa leo (yaani sisi Kizazi cha MUNGU). Maana sisi tupo hapa ikiwa wakati wa kuumiliki ufalme umewadia, na Mzee wa Siku yuko hapa kuvunja kila agano lililokuwa linasababisha usipate haki yako.

Msit.16 Pilato anamtia YESU mikononi mwa wayahudi ili wamsulubishe, nao wakampokea.

Ushuhuda
Kuna watu walionifuata toka mjini, wakasema Miaka1000, si utoke ukaanzishe Kanisa pembeni? Kwa nini unapata matatizo bila sababu? Nikasema, lakini Eliya AD2 hakuniacha pembeni! Aliniacha pale madhabahuni, mimi nitamjibu nini mbinguni (ikiwa nitaondoka hapa)? Wakasema utapata matatizo!

Sasa hawa walikuwa wanaangalia kama haya yaliyompata YESU. Pia, kuna aliyekuwa ananiombea, lakini akasema hapana, hili abebe mwenyewe; kama hali ndiyo iko hivi? Sitaki kupigwa kwa sababu ya kumuombea Miaka1000. Hiyo ilikuwa inatokea kwa sababu hakuna mwenye haki aliyekuwa amepewa hati miliki.

Huyo aliyekuwa anasema hivyo si kwamba ana kosa, sivyo. Ni kwa sababu ya hali halisi ambayo sisi sote tumefunuliwa tukaikuta. Siyo Musa aliyekosea, siyo Eliya Mtishbi, Elisha,  wala siyo YESU, Petro, Paulo, Tito au Timotheo, wala siyo Eliya AD2 MUNGU wa Majeshi aliyekosea. Ni kwa sababu wote, hata Adamu1 mwenyewe, ameumbwa tayari akakuta hana hati miliki, ingawaje MUNGU amempa, lakini tayari kule juu kulishatokea limbuko baya.

Kwa hiyo ni kosa kumwona fulani amekosea, kwa sababu kulikuwepo na limbuko hilo kwamba hakuna aliyekuwa na hati miliki. Hata ukienda kazini kwako ukaona bosi wako kama hajakupa haki yako, ujue hiyo ndiyo halisi ambayo hata Adamu1 aliumbwa akaikuta. Leo Mzee wa Siku anaivunja kwa kuwa wakati umewaidia. Wakati umewaidia ili aonyeshe kuwa yeye ndiye Mzee wa Siku; kila kitu kiko chini yake, na hakuna ambaye yuko juu yake. Kama kuna uliyekuwa umemshikilia, leo umejua kuwa hutakiwi kumshikilia yeyote. Maana mchawi halisi atajulikana, aliyekuwa anasingiziwa atajulikana. Mwizi halisi atajulikana, aliyekuwa anasingiziwa naye atajulikana. Hii ni kwa sababu Mzee wa Siku yuko yeye mwenyewe, na ndicho alichokuja kufanya ili utawala wa amani usimame (Dan.2:44), na Kanisa sasa liende kila mahali.

Katika msit.23 askari waliyagawana mavazi ya YESU mafungu manne, lakini kanzu wakaipigia kura. Hapo ndipo mashariki ya kati walichukua mavazi namna hii (meupe). Asubuhi ya leo ninamshukuru MUNGU, ni kwa kuwa sasa kila mmoja atalipwa sawa sawa na usafi wa mikono yake. Hii ni kwa kuwa MUNGU ana kurejeshea Hati Miliki ya kile Kiti cha Urithi wa MUNGU. Kwa sababu bila hati miliki ungeweza kunyang’anywa. Nakuhakikishia kwamba sasa mambo mengi yatarekebika, hata mishahara kwa wengi itarekebika. Kilichokuwa kinasababisha mambo yaende kama yalivyokwenda ilikuwa ni kwa kuwa Uumbaji wote wa MUNGU ulikuwa mikononi mwa dunia. Hii ni kwa sababu hakuna kitu kinachoitwa dunia na ulimwengu bila walimwengu kuiba kutoka kwa watakatifu. Ukisikia kuna hawa walimwengu, ni kwa sababu wameiba kutoka kwa watakatifu; ukisikia kitu kinachoitwa dunia ni kwa kuwa imeiba kutoka kwa MUNGU. Leo Mzee wa Siku anafuta kabisa agano hilo kuanzia sasa hivi. Kwa hiyo kuanzia sasa:
+ Hutaugua kwa niaba ya mwingine;
+ Hutafungwa kwa niaba ya mwingine;
+ Hutalia kwa niaba ya mwingine;
+ Hutaumizwa kwa niaba ya mwingine; n.k.

Mfano mwingine unayothibitisha hali ilivyokuwa, lakini sasa MUNGU anaondoa yote hayo asubuhi ya leo.

Yn.9:7-  Muombaji kipofu aliyeona
Neno linasema “Akamwambia nenda kanawe katika birika la Siloamu (maana yake aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona”. Huyu alizaliwa akiwa kipofu, na aliponywa siku ya sabato. Mafarisayo wanasema katika Msit.16, kwamba aliyemponya (YESU) hakutoka kwa MUNGU kwa sababu “haishiki sabato”, kwa sababu tendo hili alilifanya siku ya sabato. Lakini sabato maana yake ni kustarehe, na aliyekuwa kipofu alistareheshwa (kwa kuponywa upofu). Kukawa na faraka kati yao kwa sababu wengine walihoji kwamba, “... Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hii?” (msit.16). Hata wazazi wake walipoulizwa juu ya kupona kwa mtoto wao, hawakutaka kumsifia YESU kwani waliogopa wasije wakamsifia ambaye hana hati miliki ikawaletea shida.

Msit.35, YESU aliposikia jinsi yule aliyekuwa kipofu alivyofanyiwa na mafarisayo (walimtoa nje ya Sinagogi), alipokutana naye alimuuliza kama anamwamini Mwana wa MUNGU. Naye akasema, akimfaamu atamwamini. Ina maana kuwa hata yeye aliyeponywa alikuwa hamjui YESU.

Ushuhuda
NJIAZABWANA1 leo alipokuja kunichukua, nikamwambia hivi: Haijwahi kutokea siku nzuri kama leo. Hiyo ndiyo “Shika neno” niliyomwambia asubuhi ya leo. Yaani badala ya kumwambia “Shika Neno” nilimwambia haijawahi kutokea siku nzuri kama leo! Nikasema “hata mimi Miaka1000 kuanzia leo sitaonekana mwovu tena!” Nikamwambia, “nitaonekana mwema kama ninavyotenda mema.” Ndiyo maana nikamwambia haijawahi kutokea siku njema kama leo!
Kwa hiyo leo nakwambia hivi:
+ Kama uliwahi kusingiziwa, hutasikia tena! Mzee wa Siku yuko hapa kufuta yote haya. Kwa sababu wakati umewadia, maana MUNGU anajali sana wakati.
+ Kama uliwahi kupata hasara, hutapata tena;
+ Kama uliwahi kusingiziwa umeiba wakati waliiba wengine, hiyo kesi MUNGU ameifuta, Mzee wa Siku mwenyewe.

Ndiyo maana nikamwambia NJIAZABWANA1 kwamba hakujawahi kuwa na siku nzuri kama leo, maana hata MUNGU mwenyewe hataambiwa ni mapenzi ya MUNGU wakati ni mchawi ameua. Yaani MUNGU mwenyewe leo amepata Hati Miliki ya Uumbaji wake. Uumbaji wote umerudi kwa MUNGU yeye mwenyewe.

Hili linatokea Tokyo, Japan, linatokea Los Angels, Marekani, linatokea Capetown, Afrika ya Kusini, linatokea hata Sidney, Australia hapa ninavyoongea. Yaani swala hili halitokei kwetu sisi tu tuliopo hapa! Hata ndani ya taifa katika sekta zote. Yeyote aliyewahi kuonewa hataonewa tena.

LEO HAKI INASIMAMA KILA MAHALI!


+ Hata aliyeibiwa kichwa wake anarejea leo!
+ Hata aliyeibiwa kanisa wake anarejea leo!
Kila kitu kinarejea kwenye “line” yake. Nataka ulijue hili kwamba MUNGU AMELITENDA!
+ Hata yule aliyekuwa hawezi, sasa ataweza kutetea. Maana Pilato alijitahidi kumtetea YESU lakini akashindwa, lakini sasa angekuwapo angemtetea.

Nataka mjue kuwa “LEO NI SIKU YA KUTISHA KWA SABABU HAKI IMEKAA KWENYE LINE YAKE”.

Leo kila mmoja anaanza maisha kwa sababu kila mmoja anapokea haki yake. Kila mmoja amshukuru MUNGU kwamba:

MWENYE HAKI AMEKUWA MWENYE HAKI, NA YULE ANAYESTAHILI KUWA MWOVU, AMEKUWA MVOVU!

Haya anayafanya Mzee wa Siku mwenyewe. Mimi siwezi, ila Mzee wa Siku yeye anaweza! Hii inafanyika ndani ya kufumba na kufumbua kila mahali. Mtasikia kwenye vyombo vya habari kwamba “kila mwenye haki amepokea haki yake!!!” Kwa sababu siyo mimi ila ni Mzee wa Siku ambaye yuko kila mahali.

HITIMISHO

Katika 1Kor.6:2 Neno linasema “watakatifu watahukumu ulimwengu, na watahukumu malaika. Wakati huo sasa umefika. Kwa hiyo Dan.7:22a inakwenda na 1Kor.6:2-3a. Ni wakati wa watakatatifu kuhukumu ulimwengu na malaika. Kwa hiyo wale malaika ambao:
+ Wametumwa leo kukuletea fedha wasipokuletea leo wanahukumiwa; hivyo ni lazima walete;
+ Waliotumwa leo kukuletea haki, wasipoleta wanahukumiwa; kwa hiyo haki yako leo lazima walete;

Ujue pia kwamba Mzee wa Siku amekuja na jeshi lake yeye mwenyewe, lililoandaliwa kuhakikisha kwamba hili neno linatimia! Kwa sababu ni majira yake.

+ Wale malaika walioamriwa leo wakuletee utajiri, wasipouleta wanahukumiwa. Nao hawataki kuhukumiwa, hivyo ni lazima walete;
+ Wale malaika waliomriwa kukuletea marupurupu, lazima walete, wasipoleta wanahukumiwa;
+ Wale malaika walioamriwa kwenda kufuta mashitaka yako, lazima waende wayafute kwa sababu umesingiziwa. Wasipokwenda wanahukumiwa;
+ Wale malaika walioamriwa kukutoa kifungoni, lazima waende kukutoa kifungoni, wasipokwenda wanahukumiwa.
Hivyo MUNGU akufungue macho:
+ uone malaika jinsi wanavyokutoa vitanzi shingoni mwako sasa hivi! Wanafungua pingu kwenye mikono yako!
+ Uone wanavyotoka kusini, kaskazini, mashariki na magharibi wakikuletea utajiri wa mataifa.

Wakati roho Mtakatifu anaandika haya ndani ya Paulo alisema “Mta...”, wakati umefika ni sasa hivi! Siyo baadaye bali ni sasa hivi!

Kuna kitu kizuri ulikuwa unahitaji, ila ulikuwa na wasiwasi na mtaji wako. Sasa usiogope swala la mtaji, hilo halikuhusu wewe. Hilo linawahusu malaika ambao wanatakiwa wakachukue mtaji wanakojua wao! Nao wanaoogopa kuhukumiwa lazima waende.
Mzee wa Siku alipokuja watakatifu wakapewa kuhukumu!

+ Wale malaika wanaoongozana na Rafaeli, ambao waliagizwa leo wakaushe magonjwa yaliyokuwa yamesalia ndani yako, ni lazima wakaushe hayo magonjwa. Maana wasipoyakausha watahukumiwa.

Ungekuwa unaweza kuona rohoni ungeona jinsi malaika wanavyoshindwa kupishana ili kuhakikisha kwamba wanakutumikia wewe!

Mimi sitaki tena kusikia anayekuja kwangu analia akiniambia amesingiziwa! Leo lazima malaika wanaohusika waingie kazini!
Sitaki kusikia aliyeshitakiwa bila sababu yoyote!
Hata mimi Miaka1000 sitaki kuandikiwa barua ya kushutumiwa wakati sijakosea! SITAKI TENA! SITAKI TENA!

MIAKA 1000
Wakili wa MUNGU kizazi cha MUNGU
KUNA ANAYEFIKIRI ANANISHUTUMU MIMI KUMBE ANAMSHUTUMU NILIYEMBEBA!!

SITAKI MUNGU ASHUTUMIWE WAKATI MIMI SIJAKOSEA!!

JESHI LINALONILINDA LIINGIE KAZINI!!!