Thursday, 25 August 2016

KUVUNJA AGANO LA WENYE HAKI KUONEKANA WAOVU NA WAOVU KUONEKANA WENYE HAKI VIZAZI VYOTE


2 SHEBATI TANO

MIAKA1000 YA KUTAWALA NA KRISTO
WAKILI WA MUNGU KIZAZI CHA MUNGU


SHUKRANI

Tunamshukuru MUNGU leo ni siku ya pili katika mwezi wa ushindi, mwaka wa Uzalishaji Rohoni, Mji Mtakatifu. Tunamshukuru MUNGU kwa ajili ya somo linaloendelea, kwamba kila mmoja analipwa sawa sawa na usafi wa mikono yake. Hili siyo kwetu peke yetu bali ni ndani ya Uumbaji wote.

Nataka tumshukuru MUNGU kwa sababu hayo yanaendelea kutokea, kwamba haki yako sasa unayo na unalipwa kwa damu ya MUNGU mwenyewe. Mahali popote ambapo ulikuwa huna Hati Miliki ya baraka ambazo unatakiwa upate kutokana na safu ambayo MUNGU alikupa, sasa unaanza kupokea. Pia, kila mmoja sasa amesimamishwa kwenye safu yake, na sasa anapokea marupurupu ambayo yapo kwenye safu yake. Pia sasa unapokea hatima yako ambayo iko kwenye Hati Miliki.

Ibada zinazofanyikia hapa zinahudumia Uumbaji wote. Ni muhimu tulete vituo vyote na Uumbaji wote. Huwezi ukajua, inawezekana hatma yako ilibaki Ulaya, hivyo ni lazima tuilete Ulaya hapa ili kama marupurupu yako yalibaki huko yaje sasa hivi. Inawezekana hati miliki ya mambo yako mazuri ilibaki kwenye ukoo wako, hivyo lazima ukoo uletwe hapa ili vitu vyako vije hapa. Hivyo ni wakati wa kurejesha Uumbaji wote uwe hapa ili kila mmoja akiondoka asubuhi ya leo, aweze kupokea halali yake; afya yake; n.k.

Chochote unachotamani asubuhi ya leo ambacho MUNGU alikukusudia tangu mwanzo, leo unapokea. Maana lile agano lililokuwepo la kila wakati mwenye haki kuonekana ni muovu, MUNGU leo analivunja. Lile jambo ambapo aliyekushitaki kwa uongo ndiye alikuwa anaonekana ndiye mwenye haki, leo MUNGU analivunja mwenyewe. Kwa hiyo basi kila mmoja lazima apokee sawasawa na haja ya moyo wake. Hili ndilo agizo lililoanzisha Kanisa hili, sasa kila mmoja afurahie wokovu wa kweli. Kila mmoja afurahie kuamka kuja ibadani, na usione tena hasara.

Tunaendelea kusimama na Dan.7:22 ambayo ina sehemu mbili.
(1) Watakatifu kupewa kuhukumu
(2) Wakati umewadia watakatifu kuumiliki ufalme

Tumekwishaona kwamba hatuwezi kuumiliki ufalme wakati bila hati miliki. Kilichokuwa kinazuia wenye haki au watendao kwa mikono yenye usafi wasipokee  stahili yako, ni kwa mwenye haki  vizazi vyote kutokuwa na hati miliki ya safu yake! Hapo ndipo palipokuwa na chanzo cha mwenye haki kutopokea kile anachostahili ambacho MUNGU amemwahidi apokee. MUNGU alichofanya jana ni kila mmoja kumrejeshea hati miliki ya safu yake.

Kila mmoja ana nafasi katika jamii; katika familia mwingine ni baba na mwingine ni mama, mwingine ni mtoto; na kuna mtoto wa kwanza mpaka wa mwisho. Katika wajibu kuna ambaye ni “General Manager”, mwingine ni “manager”, kuna ambaye ni mfanyakazi wa aina fulani, na katika biashara na katika kulima kadhalika. Lakini kwa kuwa tangu mwanzo MUNGU alisogezwa pembeni na kerubi, akaondoka kwenye Mlima wake, basi ilileta limbuko kwamba kila atakayetenda kwa haki na yeye atasogezwa pembeni. Kwa hiyo ilisababisha kila anayetenda haki asilipwe sawasawa na haki yake. Hilo ndilo lililosababisha Mzee wa Siku kuja wakati ulipowadia ahukumu kwanza hali hiyo. Maagano kama hayo yaliwekewa makafara mbali mbali na yakadumu mpaka dunia ikaonekana kwamba ndivyo inavyotakiwa iwe.

Kuna maeneo mbali mbali ambayo yalikuwa yanasababisha mwenye haki yeyote, wakati wowote asiweze kuwa na hati miliki ya mahali alipo. Hivyo akawa hapokei sawa sawa na vile anavyofanya. MUNGU amekuja mwenyewe kuwa yeye ndiye aliyeumba kila kitu, na umefika wakati atuonyeshe kwamba yupo, na yeye ndiye aliyeumba kila kitu.

Juzi nilitoa mfano jinsi ambavyo ajali yoyote ikitokea, wengi wanasema ni mapenzi ya MUNGU, hata kama ni mchawi ametegesha mtego wake. Kwa hiyo MUNGU mwenyewe alikuwa anasingiziwa. Ikiwa MUNGU alikuwa anasingiziwa, ina maana mwenye haki ilikuwa ni halali yake kusingiziwa. Hicho ndicho ambacho  MUNGU amekuja kukifuta kisitokee tena. Kwa hiyo mwenye haki aendelee kuitwa mwenye haki, na muovu aitwe muovu, ili kila unachotenda ulipwe sawasawa na ulivyotenda. Sasa kila mmoja atapewa hati miliki ya kuwa kanisa wa fulani au kichwa wa fulani, au kuwa mtoto wa fulani na alipwe sawa sawa na mchango wake katika nafasi aliyonayo.

Nataka nikuonyeshe jinsi ambavyo MUNGU mwenyewe na wote waliotumwa, Kizazi cha 1, 2, 3 na 4, hawakuwahi kupewa hati miliki ya zile nafasi zao au safu zao. Matokeo yake walifanya kazi kwa ugumu mno kwa kuwa hati miliki ya Uumbaji wa MUNGU ilikuwa kwa kerubi. Hati miliki ya Uumbaji wote wa MUNGU ilikuwa kwa kerubi, ndiyo maana wote waliotumwa waliongoza kwa ugumu, na wale waliowafuata nao wakapata ugumu. Katika Lk.4:5-9 shetani anamtambia YESU kwamba akimsujudia atampa miliki yote aliyokuwa nayo maana yeye humpa yeyote kama apendavyo.
Tangu huko nyuma, hata kabla ya Mwa.1:1, hati miliki ya MUNGU ilikwenda mikononi mwa shetani. Hiyo ilisababisha agano la mwenye haki aonekane muovu, na muovu aonekane mwenye haki. Hiyo ilipelekea wale waliokuwa wenye haki wakaamua kwenda kufanya ushirikina, maana ilionekana kwamba ushirikina ndiyo kanuni (point). Leo Mzee wa Siku anavunja hii kanuni au huu mfumo wa maisha. Hakuna nabii wala mtume ambaye angeweza kuvunja hii kama siyo yeye mwenyewe.

Roho ya Eliya ya matengenezo, marejesho, upatanisho na kujenga, yenyewe iko pale pale; maana ndiyo iliyotupeleka mpaka kwa Mzee wa Siku. Kama siyo Roho ya Eliya tusingeweza kufika mahali hapo. Lakini sasa umefikia wakati lazima aje yeye mwenyewe Aliyetuma wote vizazi vyote anayeitwa Mzee wa Siku ndiye anayevunja haya maagano.

Nataka uone kilichofanyika kwa YESU ili ujue kwa nini Pilato ashindwe kumtetea YESU. Pilato aliona kabisa kuwa YESU ana haki lakini akashindwa kumtetea kwa sababu alikuwa hana hati miliki. Hapa ni kwamba, unakuta mwenye haki amekwenda mahakamani, amejitetea na wakili wake amemtetea, lakini kwa kuwa mwenye haki hana hati miliki, anafungwa.



Yn.19:1- Yaliyotokea kwa Yesu

Katika Msitari 4, Neno linasema “... mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sioni hatia yoyote kwake”. Mapema kabisa hapa tunaona Pilato amejaribu kwa utaalamu wake wote lakini ameona kuwa YESU hana hatia.  Wale wakuu wa wayahudi wakajibu msit.7 “... sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo anastahili kufa, kwa sababu alijifanya Mwana wa MUNGU”. Lakini ni kweli vitu vyote alivyokuwa anafanya alivifanya kwa kuwa ni Mwana wa MUNGU. Angalia hapa, Pilato ni kiongozi, na alijua kabisa kwamba YESU ana haki, lakini kwa sababu hana hati miliki ya safu yake, Pilato alishindwa kumtetea. Mzee wa Siku amekuja kuvunja agano hilo kwa Damu ya Aliyetuma wote vizazi vyote!

Katika Msit. 8 Pilato pamoja na kwamba ni kiongozi lakini anawaogopa wale anawaoongoza. Pilato anamtishia YESU kwamba ana mamlaka ya kumfungua au kumwacha kifungoni. Naye YESU akamjibu kwamba mamlaka hiyo amepewa kutoka juu, na kwamba aliyemtia yeye (YESU) mikononi mwake (Pilato) ndiye mwenye dhambi zaidi. Lakini kwa kuwa hati miliki imechukuliwa siku nyingi, anaishia kusema tu lakini wakamtandika tu. Yaani, kwa kuwa YESU hakuwa na hati miliki, kujua kwake kwamba hana hatia, hakukumsaidia, na hiyo ndiyo sababu Pilato hakuweza kumtetea. Lakini Mzee wa Siku amekuja kuyamaliza yote hayo.

Kinachoendelea hapo juu ni sawa na kwamba kichwa wako amechukuliwa na kahaba, na wewe ndiyo mwenye haki, lakini anaondoka unamuona hivi hivi kwa kuwa hati miliki ilikuwa haipo. Ila leo, kwa kuwa Mzee wa Siku mwenyewe amekuja ili upate haki yako, anayamaliza hayo kwa Damu ya MUNGU Aliyetuma wote.

Katika mstari wa 12, Pilato alitafuta kila mbinu kumfungua YESU, lakini wayahudi wakamwambia “... ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake na Kaisari, kila mtu ajifanyaye mfalme humfitini Kaisari”. Suala la hati miliki ni kubwa sana kuliko ambavyo unaweza kufikiria kwa safu yako. Pilato ni kiongozi aliyepewa mamlaka yote na Kaisari, na ameshaona YESU hana hatia, lakini ameshidwa kumtoa, alibaki akiwabembeleza wayahudi, na wao hawambembelezeki. Wanataka mpaka aadhibiwe. Katika msit.15 Pilato anawaambia wakuu wa makuhani “... nimsulubishe mfalme wenu?” wakamjbu “... sisi hatuna mfalme ila Kaisari”. Wakuu wa makuhani walijua kabisa kwamba huyu ametumwa na MUNGU kuja kuokoa ulimwengu, lakini wakakataa. Pilato naye alilijua hilo lakini alikuwa hana namana kwa kuwa alikuja bila hati miliki. Pamoja na hayo wakati wa kuumiliki ufalme ulikuwa haujawadia. Kwa hiyo tuna neema kubwa tulioko hapa leo (yaani sisi Kizazi cha MUNGU). Maana sisi tupo hapa ikiwa wakati wa kuumiliki ufalme umewadia, na Mzee wa Siku yuko hapa kuvunja kila agano lililokuwa linasababisha usipate haki yako.

Msit.16 Pilato anamtia YESU mikononi mwa wayahudi ili wamsulubishe, nao wakampokea.

Ushuhuda
Kuna watu walionifuata toka mjini, wakasema Miaka1000, si utoke ukaanzishe Kanisa pembeni? Kwa nini unapata matatizo bila sababu? Nikasema, lakini Eliya AD2 hakuniacha pembeni! Aliniacha pale madhabahuni, mimi nitamjibu nini mbinguni (ikiwa nitaondoka hapa)? Wakasema utapata matatizo!

Sasa hawa walikuwa wanaangalia kama haya yaliyompata YESU. Pia, kuna aliyekuwa ananiombea, lakini akasema hapana, hili abebe mwenyewe; kama hali ndiyo iko hivi? Sitaki kupigwa kwa sababu ya kumuombea Miaka1000. Hiyo ilikuwa inatokea kwa sababu hakuna mwenye haki aliyekuwa amepewa hati miliki.

Huyo aliyekuwa anasema hivyo si kwamba ana kosa, sivyo. Ni kwa sababu ya hali halisi ambayo sisi sote tumefunuliwa tukaikuta. Siyo Musa aliyekosea, siyo Eliya Mtishbi, Elisha,  wala siyo YESU, Petro, Paulo, Tito au Timotheo, wala siyo Eliya AD2 MUNGU wa Majeshi aliyekosea. Ni kwa sababu wote, hata Adamu1 mwenyewe, ameumbwa tayari akakuta hana hati miliki, ingawaje MUNGU amempa, lakini tayari kule juu kulishatokea limbuko baya.

Kwa hiyo ni kosa kumwona fulani amekosea, kwa sababu kulikuwepo na limbuko hilo kwamba hakuna aliyekuwa na hati miliki. Hata ukienda kazini kwako ukaona bosi wako kama hajakupa haki yako, ujue hiyo ndiyo halisi ambayo hata Adamu1 aliumbwa akaikuta. Leo Mzee wa Siku anaivunja kwa kuwa wakati umewaidia. Wakati umewaidia ili aonyeshe kuwa yeye ndiye Mzee wa Siku; kila kitu kiko chini yake, na hakuna ambaye yuko juu yake. Kama kuna uliyekuwa umemshikilia, leo umejua kuwa hutakiwi kumshikilia yeyote. Maana mchawi halisi atajulikana, aliyekuwa anasingiziwa atajulikana. Mwizi halisi atajulikana, aliyekuwa anasingiziwa naye atajulikana. Hii ni kwa sababu Mzee wa Siku yuko yeye mwenyewe, na ndicho alichokuja kufanya ili utawala wa amani usimame (Dan.2:44), na Kanisa sasa liende kila mahali.

Katika msit.23 askari waliyagawana mavazi ya YESU mafungu manne, lakini kanzu wakaipigia kura. Hapo ndipo mashariki ya kati walichukua mavazi namna hii (meupe). Asubuhi ya leo ninamshukuru MUNGU, ni kwa kuwa sasa kila mmoja atalipwa sawa sawa na usafi wa mikono yake. Hii ni kwa kuwa MUNGU ana kurejeshea Hati Miliki ya kile Kiti cha Urithi wa MUNGU. Kwa sababu bila hati miliki ungeweza kunyang’anywa. Nakuhakikishia kwamba sasa mambo mengi yatarekebika, hata mishahara kwa wengi itarekebika. Kilichokuwa kinasababisha mambo yaende kama yalivyokwenda ilikuwa ni kwa kuwa Uumbaji wote wa MUNGU ulikuwa mikononi mwa dunia. Hii ni kwa sababu hakuna kitu kinachoitwa dunia na ulimwengu bila walimwengu kuiba kutoka kwa watakatifu. Ukisikia kuna hawa walimwengu, ni kwa sababu wameiba kutoka kwa watakatifu; ukisikia kitu kinachoitwa dunia ni kwa kuwa imeiba kutoka kwa MUNGU. Leo Mzee wa Siku anafuta kabisa agano hilo kuanzia sasa hivi. Kwa hiyo kuanzia sasa:
+ Hutaugua kwa niaba ya mwingine;
+ Hutafungwa kwa niaba ya mwingine;
+ Hutalia kwa niaba ya mwingine;
+ Hutaumizwa kwa niaba ya mwingine; n.k.

Mfano mwingine unayothibitisha hali ilivyokuwa, lakini sasa MUNGU anaondoa yote hayo asubuhi ya leo.

Yn.9:7-  Muombaji kipofu aliyeona
Neno linasema “Akamwambia nenda kanawe katika birika la Siloamu (maana yake aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona”. Huyu alizaliwa akiwa kipofu, na aliponywa siku ya sabato. Mafarisayo wanasema katika Msit.16, kwamba aliyemponya (YESU) hakutoka kwa MUNGU kwa sababu “haishiki sabato”, kwa sababu tendo hili alilifanya siku ya sabato. Lakini sabato maana yake ni kustarehe, na aliyekuwa kipofu alistareheshwa (kwa kuponywa upofu). Kukawa na faraka kati yao kwa sababu wengine walihoji kwamba, “... Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hii?” (msit.16). Hata wazazi wake walipoulizwa juu ya kupona kwa mtoto wao, hawakutaka kumsifia YESU kwani waliogopa wasije wakamsifia ambaye hana hati miliki ikawaletea shida.

Msit.35, YESU aliposikia jinsi yule aliyekuwa kipofu alivyofanyiwa na mafarisayo (walimtoa nje ya Sinagogi), alipokutana naye alimuuliza kama anamwamini Mwana wa MUNGU. Naye akasema, akimfaamu atamwamini. Ina maana kuwa hata yeye aliyeponywa alikuwa hamjui YESU.

Ushuhuda
NJIAZABWANA1 leo alipokuja kunichukua, nikamwambia hivi: Haijwahi kutokea siku nzuri kama leo. Hiyo ndiyo “Shika neno” niliyomwambia asubuhi ya leo. Yaani badala ya kumwambia “Shika Neno” nilimwambia haijawahi kutokea siku nzuri kama leo! Nikasema “hata mimi Miaka1000 kuanzia leo sitaonekana mwovu tena!” Nikamwambia, “nitaonekana mwema kama ninavyotenda mema.” Ndiyo maana nikamwambia haijawahi kutokea siku njema kama leo!
Kwa hiyo leo nakwambia hivi:
+ Kama uliwahi kusingiziwa, hutasikia tena! Mzee wa Siku yuko hapa kufuta yote haya. Kwa sababu wakati umewadia, maana MUNGU anajali sana wakati.
+ Kama uliwahi kupata hasara, hutapata tena;
+ Kama uliwahi kusingiziwa umeiba wakati waliiba wengine, hiyo kesi MUNGU ameifuta, Mzee wa Siku mwenyewe.

Ndiyo maana nikamwambia NJIAZABWANA1 kwamba hakujawahi kuwa na siku nzuri kama leo, maana hata MUNGU mwenyewe hataambiwa ni mapenzi ya MUNGU wakati ni mchawi ameua. Yaani MUNGU mwenyewe leo amepata Hati Miliki ya Uumbaji wake. Uumbaji wote umerudi kwa MUNGU yeye mwenyewe.

Hili linatokea Tokyo, Japan, linatokea Los Angels, Marekani, linatokea Capetown, Afrika ya Kusini, linatokea hata Sidney, Australia hapa ninavyoongea. Yaani swala hili halitokei kwetu sisi tu tuliopo hapa! Hata ndani ya taifa katika sekta zote. Yeyote aliyewahi kuonewa hataonewa tena.

LEO HAKI INASIMAMA KILA MAHALI!


+ Hata aliyeibiwa kichwa wake anarejea leo!
+ Hata aliyeibiwa kanisa wake anarejea leo!
Kila kitu kinarejea kwenye “line” yake. Nataka ulijue hili kwamba MUNGU AMELITENDA!
+ Hata yule aliyekuwa hawezi, sasa ataweza kutetea. Maana Pilato alijitahidi kumtetea YESU lakini akashindwa, lakini sasa angekuwapo angemtetea.

Nataka mjue kuwa “LEO NI SIKU YA KUTISHA KWA SABABU HAKI IMEKAA KWENYE LINE YAKE”.

Leo kila mmoja anaanza maisha kwa sababu kila mmoja anapokea haki yake. Kila mmoja amshukuru MUNGU kwamba:

MWENYE HAKI AMEKUWA MWENYE HAKI, NA YULE ANAYESTAHILI KUWA MWOVU, AMEKUWA MVOVU!

Haya anayafanya Mzee wa Siku mwenyewe. Mimi siwezi, ila Mzee wa Siku yeye anaweza! Hii inafanyika ndani ya kufumba na kufumbua kila mahali. Mtasikia kwenye vyombo vya habari kwamba “kila mwenye haki amepokea haki yake!!!” Kwa sababu siyo mimi ila ni Mzee wa Siku ambaye yuko kila mahali.

HITIMISHO

Katika 1Kor.6:2 Neno linasema “watakatifu watahukumu ulimwengu, na watahukumu malaika. Wakati huo sasa umefika. Kwa hiyo Dan.7:22a inakwenda na 1Kor.6:2-3a. Ni wakati wa watakatatifu kuhukumu ulimwengu na malaika. Kwa hiyo wale malaika ambao:
+ Wametumwa leo kukuletea fedha wasipokuletea leo wanahukumiwa; hivyo ni lazima walete;
+ Waliotumwa leo kukuletea haki, wasipoleta wanahukumiwa; kwa hiyo haki yako leo lazima walete;

Ujue pia kwamba Mzee wa Siku amekuja na jeshi lake yeye mwenyewe, lililoandaliwa kuhakikisha kwamba hili neno linatimia! Kwa sababu ni majira yake.

+ Wale malaika walioamriwa leo wakuletee utajiri, wasipouleta wanahukumiwa. Nao hawataki kuhukumiwa, hivyo ni lazima walete;
+ Wale malaika waliomriwa kukuletea marupurupu, lazima walete, wasipoleta wanahukumiwa;
+ Wale malaika walioamriwa kwenda kufuta mashitaka yako, lazima waende wayafute kwa sababu umesingiziwa. Wasipokwenda wanahukumiwa;
+ Wale malaika walioamriwa kukutoa kifungoni, lazima waende kukutoa kifungoni, wasipokwenda wanahukumiwa.
Hivyo MUNGU akufungue macho:
+ uone malaika jinsi wanavyokutoa vitanzi shingoni mwako sasa hivi! Wanafungua pingu kwenye mikono yako!
+ Uone wanavyotoka kusini, kaskazini, mashariki na magharibi wakikuletea utajiri wa mataifa.

Wakati roho Mtakatifu anaandika haya ndani ya Paulo alisema “Mta...”, wakati umefika ni sasa hivi! Siyo baadaye bali ni sasa hivi!

Kuna kitu kizuri ulikuwa unahitaji, ila ulikuwa na wasiwasi na mtaji wako. Sasa usiogope swala la mtaji, hilo halikuhusu wewe. Hilo linawahusu malaika ambao wanatakiwa wakachukue mtaji wanakojua wao! Nao wanaoogopa kuhukumiwa lazima waende.
Mzee wa Siku alipokuja watakatifu wakapewa kuhukumu!

+ Wale malaika wanaoongozana na Rafaeli, ambao waliagizwa leo wakaushe magonjwa yaliyokuwa yamesalia ndani yako, ni lazima wakaushe hayo magonjwa. Maana wasipoyakausha watahukumiwa.

Ungekuwa unaweza kuona rohoni ungeona jinsi malaika wanavyoshindwa kupishana ili kuhakikisha kwamba wanakutumikia wewe!

Mimi sitaki tena kusikia anayekuja kwangu analia akiniambia amesingiziwa! Leo lazima malaika wanaohusika waingie kazini!
Sitaki kusikia aliyeshitakiwa bila sababu yoyote!
Hata mimi Miaka1000 sitaki kuandikiwa barua ya kushutumiwa wakati sijakosea! SITAKI TENA! SITAKI TENA!

MIAKA 1000
Wakili wa MUNGU kizazi cha MUNGU
KUNA ANAYEFIKIRI ANANISHUTUMU MIMI KUMBE ANAMSHUTUMU NILIYEMBEBA!!

SITAKI MUNGU ASHUTUMIWE WAKATI MIMI SIJAKOSEA!!

JESHI LINALONILINDA LIINGIE KAZINI!!!

2 comments:

  1. gibeon tunawapata vizuri but mjitahidi kuwa up to date yaani msichelewe sana kupost habari.mmebarikiwa

    ReplyDelete
  2. otherwise ufunuo wa ALIETUMA tunaupata kwa uzuri wote

    ReplyDelete